Archive for August 24, 2005

KIKWETE: Hizi si dalili njema kwetu!!!

Naam, Hii ndio Ari Mpya, Nguvu mpya na Kasi Mpya!, Haishangazi maana ukweli ni kuwa hatukuwahi kuelezwa kuwa ari hiyo, kasi hiyo na nguvu hiyo ni ya uelekeo gani na ndio maana kuna wakati nilihoji hilo ati.

Wakati CCM, ikiwa inatamba kila kona kuwa imempata mgombea ambaye ni kiboko na ‘Kiziba Mdomo’ cha wapinzani pia, imenishangaza sana kusikia kuwa jamaa huyu kipenzi cha watu ameutolea nje mdahalo uliokuwa umeandaliwa na kituo cha Televisheni cha Channel Ten.

Akiwa tayari ameshatuahidi kuwa ataendeleza yale yote mema yaliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu ambayo kauli mbiu yake ilikuwa Uwazi na Ukweli, hakika jambo la kwanza kabisa ambalo tulilitarajia wengi wetu ni kuona anakuwa wazi zaidi ya aliyemtangulia, lakini hali imekuwa kinyume. Hali hii iwe ni kutokana na shinikizo la chama au kutoka kwake mwenyewe kwakweli haiwezi kupita hivi hivi kwasababu inazusha maswali mengi kichwani mwetu.

Je, Ni mangapi ambayo mhishimiwa huyu ataamua kuyatolea nje pindi akikanyaga pale kwenye lile jumba jeupe, na je hizi ni dalili za nini au kiashiria cha jambo gani kwetu Wadanganyika??

Naam, Mwendo mdundo, Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mupyaaaaaaaaaaa!!!

August 24, 2005 at 6:38 pm 2 comments

Mbowe, Mlikuwa wapi wakati huo?

MWENYEKITI wa Chama ca Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe hihi karibuni wakati anakubali uteuzi uliofanywa na chama chake kuwa awe mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya chama hicho, alitoa risala moja ambayo ilikuwa tamu sana kuisikiliza. Tamu kwasababu kama kawaida, alijitahidi kuonyesha kiasi gani Wanasiasa wetu wanaendelea kufanya vyema katika Usanii wa kuunda maneno ili kuzidi kuwashika Wadanganyika. Katika risala hiyo kuna sehemu alisema eti :”Tanzania imemwagiwa Mafuta ya Taa na kwamba anahitajika kichaa mmoja tu ajitokeze ili kuwasha njiti na kisha italipuka (tehe tehe tehe!!!)

Inashangaza sana hakika kusikia hayo, hasa kwa mtu ambaye alinitangulia mimi kwa miaka kibao kuwasili duniani, kwasababu ukimuuliza mtu kama huyu kuwa huko awali walikuwa wapi wakati nchi inamwagiwa mafuta ya taa, utaanza kusikia longo longo za kumwaga ati. Nashindwa kuwaelewa hakika hawa jamaa zangu wanasiasa wanaposema kuwa eti hali imekuwa mbaya wakati wengi wao kama sio wote walikuwemo katika mchakato wa kuifanya hali hiyo mbaya wakati huo!

Mimi nadhani Bw. Mbowe alitakiwa kueleza ukweli kuwa Wanasiasa wetu kwa ujumla wao, walishiriki katika kuimwagia Tanzania mafuta hayo ya taa enzi hizo na sasa wanachojitahidi kufanya ni kukausha mafuta hayo japo kazi hiyo inawashinda.

August 24, 2005 at 6:16 pm Leave a comment


Blog Stats

  • 35,058 hits
August 2005
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031