Archive for August, 2005

Siku ya Blogu Ulimwenguni


Shukrani za kipekee kabisa zimwendee Mwanablogu kutoka Israel, anayekwenda kwa jina la Nir Ofir, ambaye kwa hakika wazo la kuwepo kwa siku hii lilianzishwa naye. Alionyesha kwa kiasi gani kuna baadhi ya watu humu duniani wamejaaliwa vipaji vya kufikiri na kugundua mambo ambayo katika mazingira ya kawaida kabisa hakuna wengine waliokuwa wakiyadhania.
Huyu jamaa, katika kuanzisha wazo hilo, inasemekana kuwa alikaa na kujaribu kufikiri jinsi ambavyo neno Blog linavyoweza kushabihiana na terehe fulani fulani hivi na unajua aliibuka na nini? Aliibuka na namba hii 31o8, ambayo ilimaanisha tarehe 31 ya mwezo wa nane, na baada ya hapo akapendekeza wazo hili kwa wanablogu wengine likakubalika. Hongera sana ndugu.
Pia napenda kuwapongeza ndugu zangu wengine,
Ndesanjo Macha na Maitha kwa kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kusambaza taarifa hizi katika lugha ya kiswahili.
Kwa upekee kabisa nadhani katika siku hii sitokuwa nimefanya jambo la maana sana kama sitowataja baadhi ya wanablog ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakinivutia sana kutokana na kazi zao mbalimbali, nikianza na
Bw. Reginald Simon.
Huyu kwa hakika alisimama mstari wa mbele sana katika kunishawishi kuwa mwanafamilia ya Wanablogu, na kwa hakika kazi zake zimekuwa pia ni changamoto kubwa sana kwangu katika kuboresha na kuzidi kuelimisha jamii kwa mtizamo nilionao sasa.
Kuna huyu jamaa yangu mwingine ambaye, kwakweli ukitizama kazi zake, jinsi anavyoziandika, mpangilio wa lugha yake na mpangilio wa picha zake, kwakweli utatamani kuwa kila siku uwe unaamkia kwenye Blogu yake. Namzungumzia
Akiey, ambaye unaweza kumtembelea na kushuhudia ushuhuda wangu.
Lakini pia yupo jamaa yangu mmoja anayekwenda kwa jina la Twaha Omar. Kimsingi huyu sio mzoefu sana katika ulimwengu huu lakini kuna sababu moja kubwa sana ambayo inanifanya nimhusudu na kumkumbuka kila mara, nayo ni ile ya kujituma na kujibidisha kwake kutaka kujua mambo mbalimbali ya kimaendeleo. Ukiambiwa kuwa hajawahi kuijua kompyuta hata siku moja kwa kuingia darasani, kwa hakika jamaa huyu anajitahidi na anastahili kupigwa tafu.
Wao!, Yupo Bi. Zainab Yusuph. Binti wa kwanza kabisa wa Kitanzania kuwa na blogu, yenye kumchambua mwanamke. Ingawa bado mchango wake haujaweza kuwa wa hali ya juu sana, lakini ni wazi kuwa kwa wanaofuatilia mfumuko wa Blogu za wasichana, mabinti na wanawake wa Kitanzania, watakubaliana nami kuwa yeye amekuwa sehemu ya kuwashinikiza hao kufikia hapo.
Na kwa kumbukumbu za kipekee, ningependa kuiweka katika ubongo wangu, blog mpya kabisa ambayo umri wake hadi tunaadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza, ulikuwa ni wa siku kadhaa. Hapa naizungumzia Blogu ya hili janga la Katrina lililomaliza jamaa zetu kadhaa huko Ughaibuni.
Ni wazi kabisa kuwa bado tunakabiliwa na changamoto nyingi sana mbele yetu kuhakikisha kuwa jamii inanufaika na juhudu zetu, lakini hicho kisiwe kigezo cha kutufanya tukate tamaa kwasababu naambiwa hata Rome haikujengwa kwa siku chache, achilia mbali siku moja.

August 31, 2005 at 7:16 pm 1 comment

Siku ya Kublog Duniani !!

Kuna mambo kadhaa ya muhimu sana ambayo yanajiri katika Ulimwengu wa Ma-Bloga kwa ujumla ambayo ni vyema kila mmoja akayajua. Kupitia kwa Bw. Ndesanjo Macha, nimekutana na taarifa za kuwepo kwa Siku ya Kublogi Duniani au pia waweza kuiita Siku ya Wana-Blogi Duniani. Soma zaidi kuhusu siku hiyo kwa Kiswahili HAPA. Pia soma juu ya aliyeanzisha wazo hilo HAPA.

*****************

Pia kuna Taarifa ambayo Mtanzania huyo amemaliza kuiandika kuhusu Wana-Blogi mbalimbali nchini na hata walio nje ya nchi (wenye asili ya Kitanzania, bilashaka) ambayo mnaweza kuisoma kwa kuingia katika blogi ya Sauti za Dunia (blogi ya Global Voices). Kwa mara nyingine tena, Bw. Ethan anazungumzia juu ya Wana-blogi flani flani hivi na ni vyema mkapata kile anachokisema HAPA

*************
Lakini pia kuna Wana-Blog wapya ambao wamejitambulisha rasmi katika Ulimwengu huu. Yupo huyu mmoja ambaye ameanza kwa ile staili ya Wana-CCM kuelekea uchaguzi mkuu ujao, yaani Kasi mpya, Ari mpya na Nguvu mpya. Hebu msome Bw. Swai, hapa kisha umtizame na Bw. Masare, hapa, na kisha kama ilivyo ada yetu, naamini kuwa mtawakaribisha rasmi kuungana nasi

August 29, 2005 at 8:39 pm Leave a comment

Kwa kasi hii, Hongereni Wasanii wetu.

Ingawa kwakweli bado kuna matatizo makubwa sana katika kuweka mchakato utakaowawezesha kufaidika na kazi zao, lakini kwa ujumla wanajitahidi kwa kiasi cha kutosha. Kwa ulimwengu wa sasa ambapo bisahara ni ya utandawazi, kuwa na WEBU kwa ajili ya kutangaza shughuli mbalimbali za wasanii wa Tanzania ni jambo la muhimu sana na ndio maana napenda kuwapongeza kwa kasi hii.
Kwa wale wasomaji wangu, zifuatazo ni baadhi tu ya Webu ambazo unaweza kuzipitia na ukakutana na kazi, shughuli, taarifa na maendeleo ya muziki wa Kizazi kipya hapa Tanzania au Bongo Flava, kama wanavyouita wenyewe:
Bongoflava (Hii ni kama kiongozi maana ina viunganishi mbalimbali pia kwa ajili ya kufahamu mambo zaidi ikiwa ni pamoja na habari, picha, na kadhalila), Kwetu Entertainment, Tanzaniahiphopsummit, Africanhiphop, na kwa taarifa zaidi kuhusu muziki huo unaweza kukong’oli HAPA.
Hallaaaa wasanii wa Bongo Flava!!

August 28, 2005 at 11:08 am Leave a comment

KIKWETE: Hizi si dalili njema kwetu!!!

Naam, Hii ndio Ari Mpya, Nguvu mpya na Kasi Mpya!, Haishangazi maana ukweli ni kuwa hatukuwahi kuelezwa kuwa ari hiyo, kasi hiyo na nguvu hiyo ni ya uelekeo gani na ndio maana kuna wakati nilihoji hilo ati.

Wakati CCM, ikiwa inatamba kila kona kuwa imempata mgombea ambaye ni kiboko na ‘Kiziba Mdomo’ cha wapinzani pia, imenishangaza sana kusikia kuwa jamaa huyu kipenzi cha watu ameutolea nje mdahalo uliokuwa umeandaliwa na kituo cha Televisheni cha Channel Ten.

Akiwa tayari ameshatuahidi kuwa ataendeleza yale yote mema yaliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu ambayo kauli mbiu yake ilikuwa Uwazi na Ukweli, hakika jambo la kwanza kabisa ambalo tulilitarajia wengi wetu ni kuona anakuwa wazi zaidi ya aliyemtangulia, lakini hali imekuwa kinyume. Hali hii iwe ni kutokana na shinikizo la chama au kutoka kwake mwenyewe kwakweli haiwezi kupita hivi hivi kwasababu inazusha maswali mengi kichwani mwetu.

Je, Ni mangapi ambayo mhishimiwa huyu ataamua kuyatolea nje pindi akikanyaga pale kwenye lile jumba jeupe, na je hizi ni dalili za nini au kiashiria cha jambo gani kwetu Wadanganyika??

Naam, Mwendo mdundo, Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mupyaaaaaaaaaaa!!!

August 24, 2005 at 6:38 pm 2 comments

Mbowe, Mlikuwa wapi wakati huo?

MWENYEKITI wa Chama ca Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe hihi karibuni wakati anakubali uteuzi uliofanywa na chama chake kuwa awe mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya chama hicho, alitoa risala moja ambayo ilikuwa tamu sana kuisikiliza. Tamu kwasababu kama kawaida, alijitahidi kuonyesha kiasi gani Wanasiasa wetu wanaendelea kufanya vyema katika Usanii wa kuunda maneno ili kuzidi kuwashika Wadanganyika. Katika risala hiyo kuna sehemu alisema eti :”Tanzania imemwagiwa Mafuta ya Taa na kwamba anahitajika kichaa mmoja tu ajitokeze ili kuwasha njiti na kisha italipuka (tehe tehe tehe!!!)

Inashangaza sana hakika kusikia hayo, hasa kwa mtu ambaye alinitangulia mimi kwa miaka kibao kuwasili duniani, kwasababu ukimuuliza mtu kama huyu kuwa huko awali walikuwa wapi wakati nchi inamwagiwa mafuta ya taa, utaanza kusikia longo longo za kumwaga ati. Nashindwa kuwaelewa hakika hawa jamaa zangu wanasiasa wanaposema kuwa eti hali imekuwa mbaya wakati wengi wao kama sio wote walikuwemo katika mchakato wa kuifanya hali hiyo mbaya wakati huo!

Mimi nadhani Bw. Mbowe alitakiwa kueleza ukweli kuwa Wanasiasa wetu kwa ujumla wao, walishiriki katika kuimwagia Tanzania mafuta hayo ya taa enzi hizo na sasa wanachojitahidi kufanya ni kukausha mafuta hayo japo kazi hiyo inawashinda.

August 24, 2005 at 6:16 pm Leave a comment

Uigizaji wa Wabunge wetu na hatma ya Bunge lenyewe

Nazungumzia Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kwakweli hivi sasa kuna watu wamekuwa wakijitahidi kwa kadiri wawezavyo kuhakikisha kuwa wanaufuta utukufu wake na badala yake kulifanya sehemu ya kupotezea wakati. Na HII HAPA ni moja ya kazi nyingi sana ambazo ninatarajia kuwa wasomaji wangu watashirikiana nami katika kuibua hoja za msingi kabisa za kurekebisha baadhi ya mambo ambayo ni wazi kabisa yanaenda kombo.

August 21, 2005 at 10:58 am 6 comments

Upele umewapata wenye kujua kukuna?

Kwa haraka haraka, wapo wale wenzangu na mimi ambao watakuwa wameshangazwa kama sio kushtushwa na matokeo haya, lakini ndio hivyo tena. Hayawi hayawi, hatimaye yamekua. Inawezekana kuwa yalikuwa Maajabu, kama yale ya mzee Rajabu ya kushangaa kababu akavikwa hijab, lakini ukweli utabakia palepale kuwa ndio waliopita na WENYE WIVU WAJINYONGE TU, ila wenzenu haoooooooooo, wanaingia Bungeni pale (sijui kwenda kusinzia sawa na wenzao au vipi, tuwaachie wenyewe hayo).

Kwa kutizama sifa zao tu, hakika wanastahili hicho walichokifikia. Nawazungumzia ndugu zangu hawa wawili ambao majuzi wamefanikiwa kuteuliwa kuwa wawakilishi wa vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawazungumzia Amina Chifupa Mpakanjia na mwenzake (katika uwakilishi) Lucy Thomas Mayenga. Kwa kweli kama ni kutosha kura zilitosha, lakini je ndio upele umempata mwenye kucha kweli,au kucha zimempata mwenye upele???

August 12, 2005 at 12:47 pm 3 comments

Older Posts


Blog Stats

  • 34,787 hits
August 2005
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031