Wanywaji Tanzania Mmejikomboa

June 28, 2005 at 10:48 am Leave a comment

Sijui niwasalimie kwa namna gani ndugu zangu, maana salamu nyingi sana siku hizi. Pengine wakati nikiendelea kufikiria namna nzuri ya kuwasalimia safari ijayo, naomba tuendelee na kasomo ketu ka leo maana nadhani nyote hamjambo

Kwamba Watanzania au Wadanganyika kama kaka yangu moja anayekwenda kwa jina la JK, sio yule atakayewania urahisi wa nchi, anayopenda kuwaita, hawana utamaduni wa kujisomea, inawezekana kabisa likawa suala la mjadala mkuuuubwa kulingana na na sababu mbalimbali ambazo wanaolijadili wanazo. Lakini kakwambia nani kuwa kutokusoma kwao ni tatizo linalowaumiza vichwa?

Hebu zunguka huku mitaani, hasa huku uswahilini kwetu, shuhudia wataalamu wa kutengeneza, sio kuunda au kukarabati, bali kutengeneza redio, saa, magari ya kijapani, kompyuta na vifaa vingine vya elektoriniki jiulize kuwa wamejifuzia wapi ufundi huo au wamejisomea wapi mambo hayo. Unaweza ukashangaa kuwa wengi kati yao ufundi wenyewe ulikuwa wa kurithishwa na babu zao miaka hiyo ya 47.

Lakini si ndio hao hao ambao tumekuwa tukiwakimbizia viji-luninga vyetu vinapoharibika na kisha wakavitengeneza na kuvirejesha kwetu, japo baada ya kuzungushana kwiiingi kama ilivyoa ada ya mafundi, na kisha tukaendelea kufurahia mipira ya Aseno na Manchesta utadhani na ni wamiliki wa hisa kwenye vilabu hivyo?

Ukijiuliza kwa sana utajikuta kuwa mlolongo wa maswali ni mrefu sana ilhali majibu yakiwa hayaonyeshi walau kuwa yatachomoza kichwani mwako katika siku za usoni kuhusiana na hali hiyo, lakini ukweli ndio huo, wengi wao hawajasomea mambo hayo, hawajisomei na hawana habari hiyo, ilimradi mambo yao yanaenda tu. Hii ndio Bongo bwana, kila kitu Bongo na sio vinginevyo.

Kuna jambo ambalo mimi huwa linanisumbua sana kila uchao, hivi kwa uwezo wa Bongo zao, hawa Wadanganyika wangekuwa na utamaduni wa kujisomea ingekuwa vije? Nadhani Duniani hapangekuwa sehemu yao inayowastahili, kwasababu wangekuwa mbele hata ya dunia yenyewe ati, kama huamini basi kalagabaho.

Anewei, hayo ndio maisha tunayoishi na kila ikifika jioni baada ya kutwa nzima ya kutumia Bongo, jambo la heshima sana ambalo tutaweza kufanya ni kukusanyika katika vikao vyetu vya kwenye stuli ndefu huku tukipunguza mawazo na kujipongeza.

Sijui ni kwasababu tumesamehewa madeni yetu na nchi tunazozidai kwamujibu wa kaka yangu Ndesanjo au tunafurahia nini hasa kwasababu bado tunaishi katika nyumba za kupanga, madeni lundo ya kibinafsi na kitaifa, na matatizo yakiwa ni asilimia mia zaidi ya mafanikio.

Ni katika vikao hivyo ambapo pia utabaini nguvu za huyu jamaa mwenye majina lukuki kama mmea wa Bangi. Namzungumzia Shetani, ambaye wengine pia humwita Sheitwani, Ibilisi na majina mengine mengi kulingana na mahali na hali za wanaomjadili bilashaka.

Licha ya kuwa Guni…..oh sore namaanisha Dunia, imekuwa ikimpiga vita kupita kiasi, lakini kazi hiyo inaonekana kuwa ni ngumu pengine kuliko hata ugumu wenyewe unavyoweza kuwa au kumaanisha na kama huamini basi tuulize sisi wanachama wa vikao nilivyovitaja hapo juu, vya kwenye stuli ndefu namaanisha.

Na ikiwa utabahatika kufika huko bwana ndipo hapo utakapoamini kuwa Bongo maisha hayajali kusoma wala kutokujisomea kwasababu watu wanashuka mahesabu huko utadhani wao ndio waliobuni hizo fomyula za kuyakalikuleti.

Watakupigia mahesabu ya kiasi cha fedha ambacho kinatumika katika kuhanikiza kwa mfano utamu wa Rubisi, mbege au mnazi lakini huu unaotengenezwa na jamaa zetu toka Bondeni kwa hivi sasa, maana sisi tulishindwa kutengeneza japo ni mabingwa wa kunywa, na kisha watakuuliza wapi na wapi, baada ya kulinganisha bajeti za kuhanikiza uzuri wake na zile za makundi ya wanaopinga.

“Tizama hiki wanachokiita fegi, tizama utamu wa rushwa hasa, tizama na mengine yoote yanayopigwa vita halafu linganisha juhudi za kuyapinga za kuyakubali na kuyatangaza yalivyo mazuri kisha unambie kuwa kweli kuna uwiano hapo, wewe endelea kubonyea tu bwana mdogo haya mambo mengine waachie wenyewe hii Bongo bwana kila mmoja anaishi kwa kupiga domo hata kama kwa mambo yasiyowezekana” utaishia kuambiwa hivyo

Katika kikao chetu cha juzi, ni bahati mbaya sana kuwa kamjadala hako ka nguvu za shetani dhidi ya uhalisia wa kimaisha kalikaribia kukatizwa baada ya wengi wetu kujikuta kuwa hatuna njuluku za kuweza kuzungusha raundi nyingine ya kama tulivyo, hali ambayo ilmanusura itulazimishe tuvunje kikao kwa ujumla. Lakini duh, kweli wabongo nuksi. Sio kuwa nawatukana bali nawasifia

Aliibuka jamaa mmoja ambaye nadhani pia ni miongoni mwa hawa hawa ambao shule iliwapiga chenga, au sijui ni wao waliogopa umande au vipi na kutoa wazo kama ifuatavyo: “jamani inaonekana kuwa tatizo hapa ni kuwa kila mmoja hana fedfha za kuzungusha kama tulivyo, lakini kikao kinaweza kikaendelea ikiwa na sisi tutaiga mfumo wa serikali yetu wa kukusanya nguvu zetu pamoja” jamaa akakohoa kidogo kisha akaendelea

“Unajua tunahimizwa saaana hivi sasa tuunganishe nguvu zetu katika kufanikisha mambo yetui sasa kwanini na sisi haopa watu wasijiunge walau wawili wawili kwa ajili ya kufanikisha raundi ya kama tulivyo? Na ……, jamaa hakuweza hata kumaliza maana aliibuka mwenzake ambaye utadhani alikuwa yeye ndiye mwenye kubuni mkakati huo na kudai kuwa yeye anajua zaidi hivyo aachiwe yeye ukumbi.

Si unajua tena taratibu za vikao hivi kuwa kila mwenye sauti kubwa ndiye mwenyekiti, ndiye msemaji mkuu na kuchoka kwake au kubanwa na haja ndogo ndio mwisho wa uongozi wake, basi ikawa hivyo bwana jamaa naye akasimama na kuanza kumwaga hoja zake kama ifuatavyo.

“Mimi nadhani cha msingi hapa ni kufanya juhudi za kupukutisha fedha zote za tulioko hapa kutoka mifukoni ili tulewe hata mpaka asubuhi ikibidi na ……….,” duh huyu huo ndio ulikuwa mwisho wake lakini hakukubali akataka kutumia nguvu kuendeleza hoja yake, lakini raia wema nao hawakumkubalia na ghafla mmoja wapo akaingia kwa mfuko wake na kuibuka na buku, akailaza mezani akisema kuwa huyo mshkaji alikuwa akipiga kelele hivyo akae kimya au laa ajikomboe.

Kwakuwa jamaa naye hakutaka kuonekana hana kitu, alijikakamua na kuangusha buku mbili juu ya meza na alipoanza kubwabwaja tena, jamaa mwingine akakurupuka na kuanguka dau akimtaka mtoa hoja amwagiwe bia yake kisha atondolewe kikaoni na …. na …… kamchezo kakawa hivyo hadi kutahamaki kuna fedha ya kunywa mpaka asubuhi tukaacha chenchi hapo ukumbini ili turejee jioni yake tena kuendelea na kikao.

Basi bwana kakikao ketu kakawa kamepata baraka zote za shetani kuendelea tena kwa nguvu zaidi maana fweza ipo ya kutosha, na kila raia akawa sasa anachekelea ajuavyo, wengine wakicheka kikwao, wengine kizungu, maana si unajua tena ukishajidunga kadhaa unabadilika kuwa mzungu?, ilimradi ikawa mambo juu ya mambo, hadi pale aliposimama jamaa mmoja na kuomba kuongea jambo na unadhani ni nani ambaye angemnyima ruhusa? Akapewa bwana.

“Aisee, niwashukuru saaaaana kwa juhudi za kuwezesha kikao hiki kuendelea, na kuna jambo moja la msingi kabisa napenda kuwaambia kuwa siku ya leo ni siku muhimu sana kwetu sisi wanachama wa vikao vya kwenye stuli ndefu, ni siku muhimu kwasababu ndio siku ambayo tumezindua rasmi mkakati wetu unaokwenda kwa jina la MKUFEKU” watu wote wakasikwa na butwaa, mbona walikuwa hawajui.

Jamaa akawashangaza sana alipoendelea kuwaambia kuwa uzinduzi huo umefanyika hapo hapo tulipokuwa, japo hakukuwa na mapaparaziiii na mamaraziiii, wala luninga za kuweza kuhakikisha kuwa mkakati wao unahanikizwa duniani kote na akamalizia kwa kuwauliza ni wangapi wanajua anachomaanisha, wote ziii, basi tukalazimika kumpa mji bwana na ndipo hapo alipotufunulia ukweli.

Nilikuwa namaanisha leo hii tumezindua rasmi program yetu ambayo kwa kifupi tutaiita MKUFEKU na kwa wale ambao wanataka kujua kirefu chake ni nini, basi wasijali maana yake ni Mkakati wa Kukusanya Fedha za Kulewea. Vilifuatia vicheko, vigelegele na kila aina ya mbwembwe kabla ya kuhitimishwa na wanachama wote kunyanyuka na kugonganisha glasi zao wakifanya Cheers, eti kusherehekea kuzindua mkakati wao.

Sina hakika kuwa huu utakuwa mkakati wa ngapi kati ya mingi tuliyonayo, ila nina uhakika kabisa kuwa kwa ushirikiano walionao hawa jamaa, mkakati wao huu ni wazi kabisa kuwa utadumu na sio ajabu kuwa ukapata nguvu kubwa kuliko hata ile ambayo ilishatangulia kuzaliwa kabla yake.

Nasubiri kuona kuzaliwa kwa Mkakati wa Kuchangiana Fedha za Kusomeshea Watoto a.k.a MKUFEKUWA, hivi karibuni.

Alamsiki

Entry filed under: maskani.

J.S. Malecela: Usipompenda kwa Matendo, Utampenda kwa Misimamo yake Kumbe ‘Uhishimiwa’ ni Mtamu sana

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,061 hits
June 2005
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930