Archive for June, 2005

Wanywaji Tanzania Mmejikomboa

Sijui niwasalimie kwa namna gani ndugu zangu, maana salamu nyingi sana siku hizi. Pengine wakati nikiendelea kufikiria namna nzuri ya kuwasalimia safari ijayo, naomba tuendelee na kasomo ketu ka leo maana nadhani nyote hamjambo

Kwamba Watanzania au Wadanganyika kama kaka yangu moja anayekwenda kwa jina la JK, sio yule atakayewania urahisi wa nchi, anayopenda kuwaita, hawana utamaduni wa kujisomea, inawezekana kabisa likawa suala la mjadala mkuuuubwa kulingana na na sababu mbalimbali ambazo wanaolijadili wanazo. Lakini kakwambia nani kuwa kutokusoma kwao ni tatizo linalowaumiza vichwa?

Hebu zunguka huku mitaani, hasa huku uswahilini kwetu, shuhudia wataalamu wa kutengeneza, sio kuunda au kukarabati, bali kutengeneza redio, saa, magari ya kijapani, kompyuta na vifaa vingine vya elektoriniki jiulize kuwa wamejifuzia wapi ufundi huo au wamejisomea wapi mambo hayo. Unaweza ukashangaa kuwa wengi kati yao ufundi wenyewe ulikuwa wa kurithishwa na babu zao miaka hiyo ya 47.

Lakini si ndio hao hao ambao tumekuwa tukiwakimbizia viji-luninga vyetu vinapoharibika na kisha wakavitengeneza na kuvirejesha kwetu, japo baada ya kuzungushana kwiiingi kama ilivyoa ada ya mafundi, na kisha tukaendelea kufurahia mipira ya Aseno na Manchesta utadhani na ni wamiliki wa hisa kwenye vilabu hivyo?

Ukijiuliza kwa sana utajikuta kuwa mlolongo wa maswali ni mrefu sana ilhali majibu yakiwa hayaonyeshi walau kuwa yatachomoza kichwani mwako katika siku za usoni kuhusiana na hali hiyo, lakini ukweli ndio huo, wengi wao hawajasomea mambo hayo, hawajisomei na hawana habari hiyo, ilimradi mambo yao yanaenda tu. Hii ndio Bongo bwana, kila kitu Bongo na sio vinginevyo.

Kuna jambo ambalo mimi huwa linanisumbua sana kila uchao, hivi kwa uwezo wa Bongo zao, hawa Wadanganyika wangekuwa na utamaduni wa kujisomea ingekuwa vije? Nadhani Duniani hapangekuwa sehemu yao inayowastahili, kwasababu wangekuwa mbele hata ya dunia yenyewe ati, kama huamini basi kalagabaho.

Anewei, hayo ndio maisha tunayoishi na kila ikifika jioni baada ya kutwa nzima ya kutumia Bongo, jambo la heshima sana ambalo tutaweza kufanya ni kukusanyika katika vikao vyetu vya kwenye stuli ndefu huku tukipunguza mawazo na kujipongeza.

Sijui ni kwasababu tumesamehewa madeni yetu na nchi tunazozidai kwamujibu wa kaka yangu Ndesanjo au tunafurahia nini hasa kwasababu bado tunaishi katika nyumba za kupanga, madeni lundo ya kibinafsi na kitaifa, na matatizo yakiwa ni asilimia mia zaidi ya mafanikio.

Ni katika vikao hivyo ambapo pia utabaini nguvu za huyu jamaa mwenye majina lukuki kama mmea wa Bangi. Namzungumzia Shetani, ambaye wengine pia humwita Sheitwani, Ibilisi na majina mengine mengi kulingana na mahali na hali za wanaomjadili bilashaka.

Licha ya kuwa Guni…..oh sore namaanisha Dunia, imekuwa ikimpiga vita kupita kiasi, lakini kazi hiyo inaonekana kuwa ni ngumu pengine kuliko hata ugumu wenyewe unavyoweza kuwa au kumaanisha na kama huamini basi tuulize sisi wanachama wa vikao nilivyovitaja hapo juu, vya kwenye stuli ndefu namaanisha.

Na ikiwa utabahatika kufika huko bwana ndipo hapo utakapoamini kuwa Bongo maisha hayajali kusoma wala kutokujisomea kwasababu watu wanashuka mahesabu huko utadhani wao ndio waliobuni hizo fomyula za kuyakalikuleti.

Watakupigia mahesabu ya kiasi cha fedha ambacho kinatumika katika kuhanikiza kwa mfano utamu wa Rubisi, mbege au mnazi lakini huu unaotengenezwa na jamaa zetu toka Bondeni kwa hivi sasa, maana sisi tulishindwa kutengeneza japo ni mabingwa wa kunywa, na kisha watakuuliza wapi na wapi, baada ya kulinganisha bajeti za kuhanikiza uzuri wake na zile za makundi ya wanaopinga.

“Tizama hiki wanachokiita fegi, tizama utamu wa rushwa hasa, tizama na mengine yoote yanayopigwa vita halafu linganisha juhudi za kuyapinga za kuyakubali na kuyatangaza yalivyo mazuri kisha unambie kuwa kweli kuna uwiano hapo, wewe endelea kubonyea tu bwana mdogo haya mambo mengine waachie wenyewe hii Bongo bwana kila mmoja anaishi kwa kupiga domo hata kama kwa mambo yasiyowezekana” utaishia kuambiwa hivyo

Katika kikao chetu cha juzi, ni bahati mbaya sana kuwa kamjadala hako ka nguvu za shetani dhidi ya uhalisia wa kimaisha kalikaribia kukatizwa baada ya wengi wetu kujikuta kuwa hatuna njuluku za kuweza kuzungusha raundi nyingine ya kama tulivyo, hali ambayo ilmanusura itulazimishe tuvunje kikao kwa ujumla. Lakini duh, kweli wabongo nuksi. Sio kuwa nawatukana bali nawasifia

Aliibuka jamaa mmoja ambaye nadhani pia ni miongoni mwa hawa hawa ambao shule iliwapiga chenga, au sijui ni wao waliogopa umande au vipi na kutoa wazo kama ifuatavyo: “jamani inaonekana kuwa tatizo hapa ni kuwa kila mmoja hana fedfha za kuzungusha kama tulivyo, lakini kikao kinaweza kikaendelea ikiwa na sisi tutaiga mfumo wa serikali yetu wa kukusanya nguvu zetu pamoja” jamaa akakohoa kidogo kisha akaendelea

“Unajua tunahimizwa saaana hivi sasa tuunganishe nguvu zetu katika kufanikisha mambo yetui sasa kwanini na sisi haopa watu wasijiunge walau wawili wawili kwa ajili ya kufanikisha raundi ya kama tulivyo? Na ……, jamaa hakuweza hata kumaliza maana aliibuka mwenzake ambaye utadhani alikuwa yeye ndiye mwenye kubuni mkakati huo na kudai kuwa yeye anajua zaidi hivyo aachiwe yeye ukumbi.

Si unajua tena taratibu za vikao hivi kuwa kila mwenye sauti kubwa ndiye mwenyekiti, ndiye msemaji mkuu na kuchoka kwake au kubanwa na haja ndogo ndio mwisho wa uongozi wake, basi ikawa hivyo bwana jamaa naye akasimama na kuanza kumwaga hoja zake kama ifuatavyo.

“Mimi nadhani cha msingi hapa ni kufanya juhudi za kupukutisha fedha zote za tulioko hapa kutoka mifukoni ili tulewe hata mpaka asubuhi ikibidi na ……….,” duh huyu huo ndio ulikuwa mwisho wake lakini hakukubali akataka kutumia nguvu kuendeleza hoja yake, lakini raia wema nao hawakumkubalia na ghafla mmoja wapo akaingia kwa mfuko wake na kuibuka na buku, akailaza mezani akisema kuwa huyo mshkaji alikuwa akipiga kelele hivyo akae kimya au laa ajikomboe.

Kwakuwa jamaa naye hakutaka kuonekana hana kitu, alijikakamua na kuangusha buku mbili juu ya meza na alipoanza kubwabwaja tena, jamaa mwingine akakurupuka na kuanguka dau akimtaka mtoa hoja amwagiwe bia yake kisha atondolewe kikaoni na …. na …… kamchezo kakawa hivyo hadi kutahamaki kuna fedha ya kunywa mpaka asubuhi tukaacha chenchi hapo ukumbini ili turejee jioni yake tena kuendelea na kikao.

Basi bwana kakikao ketu kakawa kamepata baraka zote za shetani kuendelea tena kwa nguvu zaidi maana fweza ipo ya kutosha, na kila raia akawa sasa anachekelea ajuavyo, wengine wakicheka kikwao, wengine kizungu, maana si unajua tena ukishajidunga kadhaa unabadilika kuwa mzungu?, ilimradi ikawa mambo juu ya mambo, hadi pale aliposimama jamaa mmoja na kuomba kuongea jambo na unadhani ni nani ambaye angemnyima ruhusa? Akapewa bwana.

“Aisee, niwashukuru saaaaana kwa juhudi za kuwezesha kikao hiki kuendelea, na kuna jambo moja la msingi kabisa napenda kuwaambia kuwa siku ya leo ni siku muhimu sana kwetu sisi wanachama wa vikao vya kwenye stuli ndefu, ni siku muhimu kwasababu ndio siku ambayo tumezindua rasmi mkakati wetu unaokwenda kwa jina la MKUFEKU” watu wote wakasikwa na butwaa, mbona walikuwa hawajui.

Jamaa akawashangaza sana alipoendelea kuwaambia kuwa uzinduzi huo umefanyika hapo hapo tulipokuwa, japo hakukuwa na mapaparaziiii na mamaraziiii, wala luninga za kuweza kuhakikisha kuwa mkakati wao unahanikizwa duniani kote na akamalizia kwa kuwauliza ni wangapi wanajua anachomaanisha, wote ziii, basi tukalazimika kumpa mji bwana na ndipo hapo alipotufunulia ukweli.

Nilikuwa namaanisha leo hii tumezindua rasmi program yetu ambayo kwa kifupi tutaiita MKUFEKU na kwa wale ambao wanataka kujua kirefu chake ni nini, basi wasijali maana yake ni Mkakati wa Kukusanya Fedha za Kulewea. Vilifuatia vicheko, vigelegele na kila aina ya mbwembwe kabla ya kuhitimishwa na wanachama wote kunyanyuka na kugonganisha glasi zao wakifanya Cheers, eti kusherehekea kuzindua mkakati wao.

Sina hakika kuwa huu utakuwa mkakati wa ngapi kati ya mingi tuliyonayo, ila nina uhakika kabisa kuwa kwa ushirikiano walionao hawa jamaa, mkakati wao huu ni wazi kabisa kuwa utadumu na sio ajabu kuwa ukapata nguvu kubwa kuliko hata ile ambayo ilishatangulia kuzaliwa kabla yake.

Nasubiri kuona kuzaliwa kwa Mkakati wa Kuchangiana Fedha za Kusomeshea Watoto a.k.a MKUFEKUWA, hivi karibuni.

Alamsiki

June 28, 2005 at 10:48 am Leave a comment

J.S. Malecela: Usipompenda kwa Matendo, Utampenda kwa Misimamo yake


“Ndugu zangu Watanzania na hasa wana-CCM, kupitia kwa wananchi wa jimbo la Mtera, napenda kuwaeleza kuwa sijaihama CCM, sio tu kuwa sitaihama CCM, bali sikuwahi katika maisha yangu kufikiria kitu hiki, hiki ndio chama kinachomaanisha kila kitu anachohitaji Mtanzania kwa ajili ya maendeleo endelevu, nitaendelea kuwa mwanachama wake, kukitumikia na nitafia CCM”

Haya yalikuwa maneno ya makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa upande wa Tanzania bara, Bw. John Samweli Malecela, alipoongea na wananchi wa jimbo lake la Mtera katika kata ya Mvumi, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza hadharani toka kuenguliwa kwake katika kinyang’anyiro cha kumsaka mgombea wa urais kwa tiketi ya chama chake.

Kauli hii ambayo ilikuja takriban mwezi mmoja toka abwagwe kwa mara ya pili katika jitihada zake za kuwania kuwa kiongozi mkuu wa Tanzania, baada ya pia kupata matokeo ya namna hiyo mwaka 1995, sio tu kuwa ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mamilioni ya Watanzania na hasa wanachama wa CCM, bali pia ilikuja katika wakati muafaka kabisa.

Ilikuja katika wakati muafaka kwasababu toka alipoenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kilichoshuhudia Bw. Jakaya Kikwete, akiibuka kidedea, kulikuwa na ubashiri wa kila namna juu ya hatma yake kiasi cha baadhi ya wana-CCM, wenzake kuanza kudhania kuwa yuko safarini kuelekea upinzani.

Ubashiri huo, ambao ulipata nguvu zaidi baada ya yeye kubwaga manyanga cheo chake cha ukamanda wa vijana, ulitokana na ukweli kuwa huyu alikuwa ni mmoja kati ya wagombea waliokuwa na nguvu kubwa sio tu ndani ya chama bali pia kwa wananchi kwa ujumla huku pia nia yake ya wazi ya kupania kushika wadhifa huo ikiwa sio ya kuhoji.

Sio hayo tu, bali pia itakumbukwa pia kuwa wakati wa mchakato mzima wa kumpata mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM, tayari ulishaenea uvumi kuwa kuna baadhi ya vigogo takriban watano ambao tayari walishafanya majadiliano na baadhi ya vyama vya upinzani juu ya wao kuhamia huko na kupewa nafasi ya moja kwa moja ya kuwania urais wa Tanzania ikiwa watakosa nafasi hiyo CCM.

Zaidi ya hayo, hata baada ya mchakato mzima kumalizika, zilienea taarifa pia kuwa makamu mwenyekiti huyo alimwandikia barua mwenyekiti wake, Benjamin William Mkapa akitaka kujiuzulu nyadhifa zote za kichama ikiwemo hiyo ya umakamu mwenyekiti, ombi ambalo hata hivyo inasemekana kuwa mwenyekiti wake alilikataa.

Iwe ni kweli kuwa tetesi hizi zilikuwa za kweli au laa, maana hazikuweza kuthibitishwa na wahusika wenyewe akiwemo mzee Malecela mwenyewe au wasemaji wa chama, jambo moja ambalo lilithibitika ni kuwa, uvumi huu ulizusha hofu miongoni mwa wana-CCM, na bilashaka kwa Watanzania wanaofuatilia masuala ya kisiasa nchini kwa ujumla wao.

Nguvu ya mzee Malecela, katika medani ya siasa nchini, ni jambo ambalo hakika sio la kuhoji kwani iko wazi kabisa na bilashaka hili ndilo lililokuwa msingi mkubwa wa shauku ya Watanzania wasio wana-CCM, kwani kuhama kwake toka chama hicho ni wazi kabisa kungeleta sura mpya katika historia ya siasa za hapa nchini.

Ndio maana mbali ya kusema kuwa ilikuja katika wakati muafaka, pia ilikuwa na umuhimu wake kwa upande wa wananchi ambao walikuwa na shauku kubwa ya kujua kuwa je, huu ndio mwanzo wa mabadiliko makubwa ya duru za kisiasa nchini au kinyume chake.

Ingawa Watanzania wengi hatujawa na utamaduni wa kutaka kushabikia mambo ambayo tunataka kujua tu kuwa yakitokea hali inakuwaje, sio siri katika hili tulisubiri kwa hamu kuona uelekeo mpya wa siasa za Kitanzania, kwani hapa dhana ambayo ingejitokeza ingekuwa ya samaki kumla mtu na sio mtu kumla samaki.

Kwa mantiki hii basi, inawezekana kabisa kuwa kilichojiri ni yale yale ya mtu kumla samaki, na hili likamaanisha kuwa hakuna lililojipya, lakini kwa hakika kauli ya mzee malecela, haiwezi kupita hivi hivi bila kujadiliwa kwa kina kwasababu inaumuhimu wake katika masuala ya kisiasa nchini mwetu.

Toka kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, takriban miaka kumi na tatu sasa, jambo moja ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara ni undumilakuwili wa wanasiasa, na hasa wale ambao wamekuwa katika nafasi za juu katika vyama mbalimbali.

Undumilakuwili huu umeshuhudia kuhama hama kwa viongozi katika baadhi ya vyama, huku wengine wakigeuza migogoro ya kuwania madaraka kama sehemu muhimu ya shughuli zao za kila siku, ilimradi kila mmoja akitaka awe katika nafasi inayomwezesha kula zaidi kuliko wengine.

Kwa ujumla jamii ya Watanzania hivi sasa imejengwa katika misingi ya kuwa, siasa ni sehemu ya kujitafutia kula badala ya kiungo muhimu sana ama injini ya kuchangamsha masuala ya kimaendeleo kama ambavyo wanasiasa wenyewe wamekuwa wakinadi kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.

Imefikia wakati ambapo wanasiasa nchini wamekuwa wakifananishwa na wasanii, kutokana na kutokuwa na msimamo. Kuhama hama vyama limekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wa kisiasa hasa kila wanapoona kuwa matarajio yao ya ulaji yanaelekea kufifishwa na watu fulani fulani.

Kutokukubaliana na ukweli kila wanapoelezana wao kwa wao au kuelezwa na wananchi, limekuwa jambo la kawaida kabisa kwa viongozi wa siasa nchini hata kama jambo wanaloelezwa wanalikiri kabisa katika nafsi zao, lakini kwakuwa nia yao sio maendeleo kama wanavyotutaka tuamini basi wamekuwa wakijitahidi hata kusaliti nafsi zao ilimradi tu wajihakikishie ulaji.

Ni kutokana na ukweli huu ndio maana naamini kabisa kuwa alichokifanya mzee Malecela, sio tu kuwa ni kitendo chenye kuonyesha ukomavu wa hali ya juu katika siasa zenye kujali demokrasia ya kweli, bali ni fundisho kubwa na darasa tosha kabisa kwa wanasiasa chipikizi na wale waliokomaa ambao wamekuwa wakiendekeza maslahi binafsi zaidi.

Ni wazi kabisa kuwa alikuwa na hamu sana na hakika alikuwa na kila sifa ya kumfanya awe sio tu mgombea urais kwa tiketi ya CCM, bali pia rais wa Tanzania, kwasababu anakila kitu kwa ajili ya nafasi hiyo, na haiyumkiniki kuwa kushindwa kwake lilikuwa linatarajiwa kuwa pigo kubwa na sababu tosha kabisa ya kumfanya atizame uelekeo mwingine wa njia anayopitia kisiasa.

Ni wazi pia kuwa kwa nguvu alizonazo, uwezo wake wa ushawishi katika jamii pamoja na ujuzi mkubwa wa masuala ya kampeni alionao, kulikuwa pia na nafasi kubwa sana kwake yeye kuhamia upinzani haraka iwezekanavyo na kisha akapewa nafasi ya kuwania urais na kisha kuibuka rais wa Tanzania kutokea upinzani.

Lakini hali haikuwa hivyo, mzee Malecela, alisahau uwezo wake wote, akaweka kando nguvu zake zote alizonazo, akazika kabisa tamaa ya madaraka, achilia mbali kuwa aliusomea hitma uvumi na bilashaka jitihada za kumshawishi kwenda upinzani na kuunyanyapaa ‘U-mimi’, na akaamua kubakia ndani ya chama ambacho kwa mara mbili kimemnyima nafasi ya kuingia Ikulu, baada ya kutumikia karibu nafasi zote za kiutendaji kichama na kiserikali zilizochini ya ile ya urais.

Kuridhika kwake kirahisi rahisi, japo kwa hakika aliamia kukubali kuwa ameshindwa, ni fundishi kubwa kwetu Watanzania wote, kuanzia wanasiasa na hasa viongozi wa vyama vya upinzani na hata wale wa CCM wenyewe kwasababu hata huko pia wapo wenye kuendekeza umimi.

Nakumbuka maneno yake ya busara sana aliyoyasema pia wakati wa mkutano alipoweka wazi hatma yake ndani ya CCM, ambapo alisema “Maendeleo ni suala ambalo haliletwi na Malecela pekeyake, bali ushirikiano wa kila mmoja wetu ndani ya chama, uwe kiongozi, mwanachama wa kawaida au mwananchi wa kawaida, kila mmoja ana nafasi yake katika kuleta maendeleo hivyo ni vyema tukaaminiana”.

Lakini hakuishia hapo maana alienda mbele zaidi hadi kuhoji kuwa inakuwaje kila mtu ajione kuwa yeye ndio kila kitu na kwamba yeye ndio pekee alistahili nafasi fulani kiasi kuwa akishindwa lazima azushe yakuzushwa ikiwa ni pamoja na kukimbilia mahakamani, kuhama chama, au mengine ambayo anakuwa anayajua mwenyewe?

“Huku ni kuonyesha kuwa una uchu wa madaraka, kwasababu kama huna uchu wa madaraka, ni wazi kuwa utakuwa ukielewa kuwa katika nafasi yoyote ile bado unaweza kushiriki katika kuleta maendeleo na tena ukiwa si ajabu na nafasi kubwa zaidi kuliko ungekuwa madarakani” aliendelea kufafanua mwanadiplomasia huyu.

Yalikuwa ni maneno mazito sana kutoka kwa mtu ambaye anazijua siasa za Tanzania na dunia kwa ujumla pengine kama ambavyo anajua kuwa yeye ni nani au ana umri gani. Ulikuwa ni ujumbe ambao sinashaka ninaposema kuwa ni changamoto ambayo wanasiasa ndani ya CCM yenyewe na wapinzani kwa ujumla wao, wanatakiwa kuichukulia kama mwongozo wa utendaji wao.

Lakini pia funzo jingine ambalo tunastahili kulichukulia kwa uzito wake kutokana na msimamo wa mwanasiasa huyu ambaye anatarajia kuwania tena nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtera ni lile la kujenga dhana akilini mwetu kuwa heshima ya mtu katika jamii haiji kutokana na nguvu alizonazo mhusika bali busara za kuweza kuchanganua mambo na kujua wakati wa kuyafanyia kazi au kuyatolea maamuzi kulingana na mahitaji.

Kwake yeye anaamini kuwa CCM, ni kila kitu, ni amani, utulivu, busara, sera zinazotekelezeka, ushirikishwaji na ushirikishaji, mshikamano, umoja na ‘kila kitu ambacho Mtanzania anahitaji’ kwa ajili ya kujihakikishia kuwa harakati zake za kimaendeleo zinafanikiwa, hivyo kuifanya iendelee kuwa madarakani ni kuwafanya Watanzania kuzidi kupiga hatua za kimaendeleo.

Je, upinzani wetu nchini umewahi kukubaliana na ukweli ndani yao japo kwa kiasi tu cha kutambua kuwa fulani ana nguvu sehemu fulani hivyo kuwekeza nguvu zao zote katika kuhakikisha kuwa chama hicho kinajiimarisha hapo?, juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa ni zile za kuhakikisha kuwa wengine nao wanajilundika hapo ili kura zigawanywe jambo ambalo limeshuhudia kuanguka kwao daima.

Kwa hakika kuna mengi sana ya kujifunza kutokana na msimamo wa mzee Malecela alioutoa hivi karibuni, iwe kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, wale wa chama tawala na hata wananchi wa kawaida pia na ni wazi kabisa kuwa kama watanzania tukiacha ile dhana ya u-mimi, ya kila mmoja kujiona kuwa yeye ndio anajua zaidi, basi kupitia somo alilotupa mzee huyu, tutakuwa katika uelekeo wa kukomaa kisiasa.

Inawezekana kabisa kuwa wapo wanaomchukia kutokanana na mapungufu yake yeye kama yeye, na hilo halishangazi kwakuwa yeye sio malaika bali binadamu, ambaye kukosea au kuwa na mapungufu sio ajabu hata kidogo, lakini hata kama mzee Malecela ni baniani mbaya, lakini kiatu chake hakika ni dawa.

…mwisho…

June 27, 2005 at 7:45 pm 3 comments

Hivi hawa wachunga kondoo vipi ?

Kama ulidhania kuwa hawa jamaa wanafanya kazi moja, basi ulikosea sana kwa maana wanachunga hadi vile visivyotakiwa kuchungwa kama huyu jamaa alivyofanya. Je kwa mwenendo huu tutafika kweli, au dunia ndio inaelekea tena kule kule kwenye enzi za Sodoma na Gomora??

June 27, 2005 at 7:23 pm Leave a comment

Hivi hawa wachunga kondoo vipi ?

Kama ulidhania kuwa hawa jamaa wanafanya kazi moja, basi ulikosea sana kwa maana wanachunga hadi vile visivyotakiwa kuchungwa kama huyu jamaa alivyofanya. Je kwa mwenendo huu tutafika kweli, au dunia ndio inaelekea tena kule kule kwenye enzi za Sodoma na Gomora??

June 27, 2005 at 7:23 pm Leave a comment

Nitablogi kongamano la BlogHer

Orodha ya wana-blogi watakaokuwa wakiblogi moja kwa moja kongamano la akina mama wenye blogi, sasa inapatikana hapa, na ninafurahi kuwaeleza kuwa nami nitakuwa mmojawapo.

June 23, 2005 at 1:05 pm Leave a comment

Majibu yangu yako tayari

Wapendwa vijana wenzangu, mabibi na mabwana, napenda kuwaambia kuwa hatimaye majibu yangu kuhusiana na afya yangu kama ambavyo niliahidi kuwa nitawataarifuni nikitoka Angaza, yako tayari na niko tayari kuyapandisha hapa wakati wowote, lakini kabla sijafanya hivyo, naomba kwanza tushirikiane kufanya hili.Naomba kila mmoja wenu ajaribu kuotea kuwa yamekuwa ya namna gani na kwanini yamekuwa hivyo unavyodhania wewe, na unanishauri nini kutokana na majibu unayodhania kuwa nimepewa huko??

June 23, 2005 at 12:36 pm 1 comment

Kila unachohitaji kiko hapa

Hii ni nzuri zaidi kwa waandishi wa habari na wanafunzi na kwa ujumla jamii ambayo imekuwa na shauku ya kutaka kujua historia au wasifu wa mataifa mbalimbali duniani. Mambo yote haya yanaweza kupatikana hapa.

June 20, 2005 at 11:51 am Leave a comment

Older Posts


Blog Stats

  • 34,787 hits
June 2005
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930