Ushindi wa Kimbunga na dhana ya Mizengwe

May 6, 2005 at 6:47 pm 2 comments

HAKUNA lililo la ajabu kwa hakika, haya ni mambo ambayo kila mtu alikuwa akiyatarajia kuwa yatatokea na kama wewe hukuwa mmoja wapo, bilashaka hukuwa sehemu ya Tanzania, na sio ajabu kuwa hata sasa haujawa hivyo. namaanisha mazungumzo na majadiliano yaliyoenea kila pembe ya Tanzania na hata nje ya Tanzania yenyewe. mazungumzo ambayo yametawala vinywani mwa watu kuhusiana na kile kilichojiri baada ya Chama tawala nchini humu (CCM), kumtangaza Bw. Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa ndiye mgombea wao wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Wapo ambao wamekuwa wakimjadili yeye kama yeye, kuwa atafanya nini baada ya kuibuka na ushindi huo ambao ulipewa jina la “Ushindi wa Kimbunga”, wapo ambao bado wangali wakijadili zoezi zima la kumpata lilivyokuwa, wapo ambao wamekuwa wakiwajadili wale walioanguka katika kinyang’anyiro hicho, wapo wengine ambao bilashaka hawafanyi lolote lile, kwa maana hawa ni wale ambao wameshakata tamaa na uongozi wa nchi hii, kutokana na sababu mbalimbali.
Mmoja kati ya hao, ni rafiki yangu mmoja ambaye ninamtambua kwa jina la Kessy Inno, ambaye alinitumia maoni baada ya kuutaarifu umma kuwa hatimaye moshi wa kijani umefuka mjini Dodoma na kumtoa Kikwete. Rafiki yangu huyu, katika maoni yake alisema kuwa yeye wiki moja kabla ya Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa tanzania, hajatangazwa kuwa mshindi, alikuwa ametabiri kuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Fredrick Sumaye, ndiye angeshinda.
Sijui kama rafiki yangu huyu alifikia kuwekeana dau la fedha au amana yoyote ile na mtu (kwasababu huwa yanatokea haya), kiasi kwamba akawa kaingia hasara kubwa kwa mgombea aliyemdhania kukosa nafasi hiyo au laa. Kama alifikia hatua hiyo basi naomba kwanza nimpe pole nyingi na baada ya hapo niingie katika kujadili maoni yake.
Katika maoni hayo, alisema kuwa yeye alidhani kuwa Bw. Sumaye ndiye angekuwa mshindi, lakini ikawa sivyo na akaniuliza mimi (kwakuwa nilikuwa na niko Dodoma), kuwa ilikuwaje hadi matokeo yakawa hivi? Kwamba kulikuwa na MIZENGWE ya namna fulani au namna gani vipi. Ni maoni haya ambayo hakika yalinivuta kuandika makala hii, kwasababu sikuwa labda na mpango wa kujadili hili neno katika siku za karibuni.
Neno hili MIZENGWE, ni neno ambalo limekuwa likizidi kujizolea umaarufu sana hususan katika medani za kisiasa nchini Tanzania, ingawa kimantiki limekuwa likimaanisha aina fulani ya mchezo mchafu. Ni neno ambalo limekuwa likitumiwa sana na viongozi wetu wa Kisiasa nchini katika kueleza jambo fulani lisilo zuri ambalo wamekuwa wakifanyiwa ama na wananchi wao au na wapinzani wao hasa katika nyakati za kugombea uongozi huo au katika kuwaondoa baadhi ya viongozi ambao huwa wanaonekana kuwa hawafai.
Sina hakika kama kweli haya ndio matumizi yake sahihi au laa lakini ninachokifahamu zaidi ya hapo ni kuwa, naamini sio rafiki yangu Inno tu ambaye aliweza kulinasibisha neno hilo na mchakato mzima wa kuelekea kupatikana kwa Bw. Kikwete. Naamini wapo wengi ambao watakuwa wakiwaza aina ya mawazo ya rafiki yangu huyu, hasa wale ambao walikuwa wamekunywa maji ya bendera za kuhakikisha kuwa watu wao wanapita na hatimaye mambo yakawa kinyume. lakini je ni kweli kuwa kulikuwa na mizengwe?
Napenda nikiri jambo moja kuwa, katika maisha yangu siamini kuwa nitakuja kuwa na kiongozi ambaye ninamuamini, kumheshimu na kumhusudu katika medani za kisiasa kama nilivyokuwa kwa hayati baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa wale watakaopenda kujua ni kwanini, naweza kutumia fursa nyingine kueleza hili, ila kwa leo napenda kusema kuwa, pamoja na kumhusudu kwa kiasi hicho, bado siwezi kukaa kimya kwa baadhi ya mamo ambayo naamini kabisa kuwa kwa kiasi fulani au kwa ujumla alifeli katika kuyatekeleza.
Naam, kama kuna mambo ambayo mzee wetu huyu alifeli kwa kiasi kikubwa kulitekeleza, basi kutokujenga mfumo wa kuelezana ukweli unaokubalika ndani ya CCM, lilikuwa moja wapo kati ya mambo hayo, hali ambayo imepelekea sehemu kubwa ya kizazi cha watanzania kukua katika mazingira hayo, kwamba mtu akikwambia ukweli amekutendea dhambi kubwa tena isiyosameheka. Matokeo ya hali hiyo kwa hakika nadhani ndio yaliyozaa, kulikuza na hatimaye kulifanya liwe endelevu neno hili MIZENGWE.
Kwa muumini yeyote yule ambaye anaamini katika kusema ukweli, nadhani kuwa hatoshindwa kukubaliana nami kuwa ni wazi kabisa kuwa kati ya wana-CCM, 11 waliokuwa wamejitokeza kwa ajili ya kuwania nafasi aliyoipata Bw. Kikwete, kwa kununua fomu kwa kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni moja, wapo ambao walikuwa wamefanya hivyo kwa ajili ya kujitangaza, wapo ambao walifanya hivyo kwa ajili ya kujifurahisha, wapo ambao walikuwa wamepania kweli kweli na wapo ambao walikuwa pengine hawajui hata walifanyalo.
Kumekuwa na huu msemo kuwa eti idadi hiyo ilimaanisha kuwa kuna kuimarika kwa demokrasia ndani ya CCM, lakini ni nani ambaye anaweza kunithibitishia kuwa kuwa na wagombea wengi huku mkiwa mnamtaka mmoja ndio kukua kwa demokrasia ndani ya chama, taasisi au kokote kule?
Mimi naamini hali hii ilitokana na kutokuwepo kwa hali ile ya kuweza kuelezana ukweli. Kwasababu kama ingekuwepo, ingewezekana kabisa wakawepo wagombea wengi zaidi ya hao lakini wenye mantiki na wanaojua kabisa kuwa wana nafasi ya kushinda kutokana na ushujaa wao waliolitendea taifa hili na wananchi wake.
Ungekuwepo utaratibu huo naamini kabisa kuwa baadhi yetu wangeliweza kabisa kutumia hizo milioni zao kwa ajili ya kuchangia hata ujenzi wa shule kwasababu walikuwa sio watu wenye uwezo wa kuwania nafasi hiyo. Mmoja kati ya wanaowania nafasi hiyo aliwahi kuwaambia watu kuwa “Ikulu sio maabara kwa ajili ya watu kwenda kufanyia majaribio”
Wapo watu ambao kutokana na mwenendo wao tu walikuwa wakijitambua wazi kuwa hata wangezikiri makaburini, bado ingekuwa shida kupita, wapo ambao walikuwa wanaelewa wazi kuwa hata kama watakesha wakisali na kuomba, bado hata Mungu asingeliweza kuwapatia fursa hiyo kwasababu yuajua mapungufu yao na hayuko Tayari kuona Watanzania wakifanywa Wadanganyika zaidi ya hapo walipofikishwa, na wapo ambao walielewa kabisa kuwa walikuwa wamefanya hivyo tu kwa lengo la kuwafanya walionuna wacheke, au kuwakoga marafiki zao kuwa kumbe wanaweza.
Wote hawa walikuwa wakifahamu haya, lakini ni nani ambaye angethubutu kuwaambia ukweli kuwa “Hii ni Taasisi ya Urais na sio Taasisi ya Urahisi, Maigizo au Ubao wa Matangazo kwa ajili ya watu kukujua kuwa wewe ni nani?, Thubutu!!, Hakuna ambaye angeliweza kusema hivyo sio tu nje ya CCM, bali hata ndani ya Chama chenyewe kwa kuhofia kuambiwa fulani ananipiga zengwe ili yeye apate.
Tuliyashuhudia haya wakati wakiranda mikoani kwa ajili ya kusaka wadhamini 25, kila mkoa (sina hakika kama kweli mkoa watu 25, wanaweza kubeba mtizamo wa mkoa mzima), ambapo kila kukicha tulikuwa tukisikia madongo kutoka kwa mmoja wao kwenda kwa mwingine, huyu akisema hili yule atasema vile ilimradi zilikuwa mbwembwe za aina zake katika wakati huo. Upo ukweli kuwa baadhi ya tuhuma zilikuwa za kipuuzi na za kuchafuliana majina hasa kwa watu waliokuwa wakiwania nafasi ya juu kama hiyo ambayo inahitaji busara za hali ya juu, lakini pia upo ukweli kuwa baadhi ya tuhuma hizo zilikuwa za msingi na zenye kuhitaji kujadiliwa. Ni nani alizijadili kati yao?
Mambo haya yaliendelea hadi wakati wa uchaguzi na hadi sasa yametangazwa matokeo ambapo ni mmoja tu kati yao ameshinda, naamini wapo ambao japo hawatokiri hadharani, lakini wataendelea kuamini hadi siku ya kufa kwao kuwa walienguliwa kwa mizengwe. lakini je ni kweli kuwa walienguliwa kwa mizengwe, mizengwe ni nini hasa na kwanini ilelekezwe kwako.
Hebu naomba mmoja wapo ajitokeze hapa aniambie kuwa ni kwanini aliamini kuwa ni lazima angelishinda pengine tutajadili hili kwa ufasaha na ukamilifu zaidi kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania, ambao wanaamini kuwa kuna mizengwe na wale ambao hatuamini kuwa kuna kitu kama hicho bali hutumika kama kivuli cha baadhi ya watu kujikinga ili kufika wanapotaka wakiwa wameloa damu, lakini pa wakitushurutisha sisi tuamini kuwa wanaowataka wakaoge wanawafanyia mizengwe.
Hongera Kikwete, Hongera CCM, Hongera wagombea mlioshindwa na Hongera kwa watanzania kwa kumfagilia Kikwete.

Entry filed under: maskani.

Hatimaye moshi wa kijani wafuka Dodoma Wasomi wetu na dhana za Kizungu

2 Comments Add your own

 • 1. Anonymous  |  October 19, 2005 at 6:07 pm

  Hey nice info you posted.
  I just browsing through some blogs and came across yours!

  Excellent blog, good to see someone actually uses em for quality posts.

  Your site kept me on for a few minutes unlike the rest 🙂

  Keep up the good work!

  Thanks!.

 • 2. banner ads  |  October 26, 2005 at 4:25 am

  There is alot of Blogs, I never guessed I’d find some usefull information.

  Thanks.
  I’ll be back later to see if anymore good updates are available.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
May 2005
M T W T F S S
 1
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
3031