Kwa vatikani ni moshi, Chimwaga zitakuwa Cheche

April 25, 2005 at 6:54 pm Leave a comment

AWALI sikuwa na nia ya kuzungumzia lolote lile kuhusiana na kikao cha ‘makadinali’ wa CCM, hasa kutokana na ukweli kuwa kuna watu kadhaa ambao ni marafiki zangu ambao wamezungumzia matarajio na hata mitizamo yao. Lakini kutokana na wingi wa maswali kutokka kwa wasomaji wangu, nimelazimika kuandika japo kiasi kidogo tu kwa lengo la kuwafurahisha, ikiwa ni ndio shukrani ya pekee niwezayo kuwapatia wasomaji wa blogu yangu.

Kuna marafiki na wasomaji wangu kadhaa ambao wamekuwa wakiniuliza kupitia mtandaoni, kuwa ni kitu gani hasa ninatarajia wakati jopo hilo la ‘makadinali’ wa ‘Chama kinachoshikilia Utamu’ watakapokutana pale katika jumba la Chimwaga kwa lengo la kumteua ‘papa’ wao kati ya 11, walionunua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo muhimu.

Kimsingi, mimi kama mwanahabari, na mdadisi wa masuala ya kisiasa hapa nchini kwetu, nadhani kwanza kuna jambo moja ambalo ningependa wasomaji wangu walitambue kuwa, kamwe sitarajii kuwa pale Chimwaga Complex, kutafuka moshi. Sio mweupe wala sio wa kijani au wa njano, au mseto wa rangi zote hizo. Katu sitarajii kuwa kutafuka moshi pale Sustine ya wana-CCM.

Kwa kuzingatia ukweli kuwa, utamaduni ambao umejengeka nchini Tanzania kwa sasa, ni ule wa chama kilichoko madarakani kuendelea kushikilia hatamu kwa muda zaidi kwa kadiri iwezekanavyo, ni wazi kabisa kuwa moja kati ya mambo ambayo watahakikisha kuwa wanayafanya ni pamoja na kuhakikisha kuwa, ‘papa’ wao ambaye watamteua, anakuwa mwenye kukubalika kwa umma wa watanzania, hata kama chama chenyewe hakikubaliki kwa kiasi hicho.

Lakkini hiyo sio sababu pekee inayonifanya niamini kuwa kitakachofuka Chimwaga, sio moshi bali zitatoka cheche zenye mchanganyiko wa rangi za njano na kijani. Chukulia kwamfano mchuano uliopo baina ya wapinzani hao 11, katika kuwania nafasi hiyo, ingawa wapo kadhaa ambao tayari watu kutokana na mitizamo yao wameshaanza kuwaengua katika kinyang’anyiro. (Hawa ni ‘sehemu ya mapadre’ ambao kimsingi huwa hawahusiki kabisa katika uteuzi huo hata hivyo)

Hilo linamaanisha wazi kuwa vyovyote iwavyo, huyu ‘Mtakavitu’ au ‘papa’ nani sijui atakuwa, atapatikana katika mazingira ambayo sio tu kwamba yatalazimu kupitishwa kwa mizengwe ya aina yake, bali pia jitihada za kila aina ikiwezekana hata kuwashirikisha ‘Sangoma’ kadhaa.

Nimelazimika kuamini kuwa jitihada zitakazofanyika zitakuwa ‘za kufa mtu’ kutokana na ukweli kuwa, kimsingi hakuna kati ya hao 11, ambaye amevunja masharti yale 13, waliyojiwekea watendaji (sijui waliwakilisha wanachama wao wote au vipi), wakuu katika chama chao.

Tukiachana na hayo, kuna huu upande mwingine, wa baadhi ya ‘makadinali’ wenye kuwania kuteuliwa kuwa ‘mapapa’, ambao inasemekana kuwa wameshaanika nia yao ya kuja kuhamia rasmi upande wa upinzani ikiwa mikutano hiyo ndani ya Sestine ya Chimwaga, itawabwaga chini. Kwa mantiki hii basi ni wazi kabisa kuwa kama watatekeleza hilo, na kufumba macho na masikio na kutokutishiwa na kauli ya katibu wao mkuu, ni wazi kabisa kuwa kitakachotokea siku hiyo sio moshi.

na unajua nini ndugu yangu, wapinzani nao wamekaa mkao wa kula tayari tayari wakisubiri ni nani atabwagwa chini ali wao wamdake kusudi awasaidie katika harakati zao za kuingia ndani ya lile jumba jeupe pale jijini Dar. Inawezekana kabisa kukawa na watu wa aina hiyo, ambao wataanguka na kisha wakaamua kufuata uelekeo wa ‘kadinali Kiraracha’ ambaye enzi zake aliamua kujitenga na kuanzisha kanisa lake lakini likawa na mafanikio duni kila kukicha.

Imani yangu inaniambia kuwa, kwa vile CCM, wanataka mtu ambaye kwa vyovyote vile, atakuwa mwiba mchungu kwa wapinzani na kukiwezesha kurudi katika jumba jeupe, ni wazi kabisa kuwa hawatotaka kutumia kuni zisizokauka vyema na kuishia kutoa moshi, bali watataka kutumia kuni madhubuti na zilizokauka uzuri ili kutoa moto mkali kuwaunguza wapinzani wao.

Na kwa upande mwingine, kama kweli hizi tetesi tetesi za mtu atakayebwagwa kuwa atakimbilia upinzani, zitatimia ni wazi kabisa kuwa kitakachozalishwa au kufuka Sestine ya Chimwaga sio moshi, bali utakuwa moto ambao si ajabu ukakiunguza CCM, katika uchaguzi mkuu ujao.

Nafunga pazia hili kwa kuwatakia kila lakheri wasomaji wangu pamoja na ‘Wadanganyika’ wenzangu kokote waliko duniani. Mungu atujaalie uhai ili tuweze kumshuhudia ‘Baba Mtakavitu’ Fulani bin Fulani, sijui wa ngapi vile.

Alamsiki

Entry filed under: maskani.

Kwa wapinzani wangu katika soka Kwa vatikani ni moshi, Chimwaga zitakuwa Cheche

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
April 2005
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930