Archive for December, 2006
Tuna UHURU lakini mbona hatuko Huru
Uzuri wa maisha na hasa kwa watu kama mimi ni kuwa falsafa ya KUCHELEWA huwa inatupitia mbali sana ndio maana hatuoni taabu kuanza kuzungumzia mambo ambayo kwa wengine tunaweza kuonekana tulishachelewa kuyazungumzia. Kwanza kuchelewa katika maisha ni nini hasa? Unawahi kwenda wapi katika maisha kwani? Anyway, tuyaache hayo tuingie katika somo la leo.
Hivi karibuni, Tanzania ilisherehekea (Sio kuadhimisha), kutimiza kwake miaka 45 toka ilipojikomboa katika ukoloni wa mwingereza. Kwakweli sherehe za mwaka huu zilifana sana na atakayekataa kwakweli hatunabudi kumwangalia kwa jicho la umakini maana hatutakii mema.
Ndege zilizungyuka angali kwa mbwembwe nyingi tofauti na hata siku tulipopata uhuru. Kulikuwa na idadi ya kutosha tu ya waliohudhuria sherehe zile pengine kuliko hata siku tuliyoutwaa uhuru huo na kwa kweli kulikuwa na kila kitu ambacho hakika kilijiri kwa mara ya kwanza. Hata maandalizi yake yalikuwa tofauti na miaka iliyopita.
Watu safari hii walishirikishwa (sio kushurutishwa?) kuchangia sherehe za miaka 45 ya uhuru wao (ah!! si ajabu lakini maana siku hizi miongoni mwa pati zinazoongoza kwa kuchangiwa michango mikubwa ni zile za kuizaliwa akina fulani) Na watu walichanga, wakachanga weee, hadi mafanikio yale tuliyoyashuhudia kwenye luninga siku ile. Kwa walioweza kuhudhuria au kuona mambo makubwa yaliyojiri siku ile, sinashaka waliondoka na picha ambayo haielezeki kwa ubora na uzuri wake. lakini Je, ni kweli tulionyesha picha yetu halisi?
Hayati baba wa taifa hili ambaye pia ndiye aliyetutoa huko mikononi mwa wakoloni na leo hii tukijiita kuwa tuko huru, Mwl. J. K. Nyerere, alikuwa akiamini kuwa “Uhuru wa mwanadamu ni uhuru ikiwa mtu huyo anakuwa huru dhidi ya Umasikini, Uonevu, Ukandamizaji, Maradhi, Ujinga huku akiwa na fikra za Umoja” Naam, ni imani hii ya mwalimu ambayo leo hii ilinisukuma kukaa na kuanza kutafakari juu ya mbwembwe za Disemba 9 2006 na hatma yetu.
Sote tunajua wazi kuwa kipindi kile Tanzania inapata Uhuru, mbali ya kuwa kwa ujumla nchi ilikuwa masikini sana, hali ya uchumi haikuwa mbaya kama ilivyo sasa ambapo tumekuwa tukishuhudia kuporomoka (Mrema anasema kuserereka) kwa fedha yetu dhidi ya fedha za nje ikiwemo hata Kenya tu ambayo wakati ule wa uhuru shilingi yao ilikuwa sawa na yetu.
Kasi ya umasikini imekuwa ikizidi kuongezeka kwa Watanzania kila uchao na hadi leo hii idadi ya wananchi wanaoendelea kuwa masikini ni zaidi ya mara tatu ya wale wanaoonyesha dalili za kunyanyuka, ukiachilia mbali lile genge la wateule fulani fulani ambao nisingelipenda kuwazungumzia hapa sababu hoja ya kujieleza walikotoa utajiri wao haijajibika mpaka sasa.
Masimulizi ya kukua kwa pato la Mtanzania ambayo yameendelea kuwa wimbo wa kila kiongozi yameendelea kutokuwa na uwiano halisi na maisha ya hao wanaoambiwa pato lao kwa mwaka limekua. Bado wangali wakilala na njaa wengi wao, bado wanaendelea kufa kutokana na kukosa huduma sababu ya kukosa fedha, wapo wanaoendelea kuwa wajinga sababu wameshindwa kulipia masomo yao na wapo ambao ah!! acha tu.
Hivi Mtanzania huyu kwa falsafa ya Nyerere juu ya Uhuru, alikuwa na kipi cha kujivunia katika siku ile, tena cha kusherehekea? Rushwa, amekuwa mdudu ambaye kila anayeingia madarakani anauimba lakini akashindwa kuucheza.
Wangali wapo Watanzania wanaokosa haki zao za msingi sababu ya rushwa, wapo wanaopoteza maisha yao sababu ya ufisadi, wapo wanaokosa hata sauti za kusemea sababu ya rushwa. Uonevu bado ungalipo, Leo hii Watanzania wangali wanachapwa bakora sababu ya kuuliza kiongozi swali. Uhuru uliopo hapo wa kusherehekea ulikuwa upi ikiwa bado uonevu unatawala hapa nchini?
Najua wapo watakaonyoosha vodole na kuhoji huyu mwandikaji wa hapa ana akili kweli? Anyway, hilo si suala langu maana madaktari ndio watakaoweza kusema kuwa ninazo au laa, lakini uwezo wa kufikiri ninao. Hivi tunajua kuwa siku ile wakati mamilioni wakiwa wanasherehekea siku ile, kulikuwa na mamilioni wengine wangapi wako kwenye njaa na mateso makubwa kutokana na kukosa huduma za msingi?
Tunajua kuwa wakati wengine walikuwa kule Uwanja wa Taifa kuna vijana wetu ambao walikuwa hata hawajui cha kufanya sababu ndoto zao za kuendelea na masomo zimekufa baada ya kukosa fedha za kujiendeleza?
Yaani ilikuwa falsafa ile ile ya uswahilini ambayo wanahabari wameipigia kelele weeee mpaka sasa wameamua kujiunga nao baada ya kushindwa kujitenga na kuwarekebisha. Nazungumzia falsafa ya kuchangishana, kuonyeshana ufahari wa shereheni lakini si katika masuala ya maendeleo, mbona walipotoswa wanafunzi pale mlimani sababu serikali haina fedha hatukutangaziwa kuchangishana kidogo kidogo ili kuweza kuwakusanyia fedha za kuwawezesha kusoma?
Ni kweli kuwa tulielezwa mambo meeeeengi sana siku ile ambayo tulitakiwa kujivunia, lakini je yanaendana na umri huo kweli? Na hawa walioko sasa wana mikakati ipi kwa ajili ya baadae maana sio suala la miaka mingine 45 ijayo tuje kuendelea kuambiwa eti taifa letu bado changa, ni kweli lakini hata watoto huwa na ndoto zao na ndoto zao wao huzitekeleza kwa matendo sio kwa maneno na porojo nyingi.
Vifo vitokanavyo na uzazi vingali vikimaliza maisha ya mama zetu, milipuko ya magonjwa ingali ikitesa wananchi wetu tena hata hapo Dar ambapo ndio kila mtu anataka kukaa hapo, kasi ya wasiokuwa na ajira nayo imekuwa ikiongezeka kila siku kutokana na sera mbovu katika mfumo wa elimu na mfumo mbovu katika kuandaa vijana kwa ujumla na kuwapa uwezo wa kulitumikia taifa lao. Huo uhuru wetu katika hali kama hii tunaweza kuuthamanisha kwa kiasi gani?
Nijuavyo mimi ni kuwa thamani ya kitu chochote ni pale kinapoonyesha matunda mazuri kama ambavyo nilitarajia kwa upande wa thamani ya uhuru wetu. Kwamba kwa kadiri ambavyo nchi ingekuwa ikipiga hatua za haraka haraka kimaendeleo kwakuwa tuna kila kinachohitajika kwa ajili ya kuendelea, basi ndio na uhuru wetu pia unazidi kuwa na thamani. LAkini tunachokifanya sasa ni kushusha thamani kama tulivyofanya kwenye fedha yetu.
Badala ya kuendelea tumekuwa ama tumesimama palepale au tunarudi nyyuma zaidi. Uhuru wetu umekuwa ni kwa manufaa ya wachache kuwaibia wengi, wachache kuwaonea wengi, wachache kudhulimu haki, fursa na maslahi ya wengi. Uhuru wa namna hii si uhuru, Uhuru wa namna hii hauna manufaa na wala hauwezi kusherehekewa kwa dhati na mbwembwe za kila aina na badala yake siku hiyo pengine ilitakiwa kutumiwa kwa ajili ya kuhitimisha labda zoezi la kukusanya kura za maoni za wananchi kuhusu mfumo bora wa elimu, mfumo bora wa kutokomeza rushwa na kadhalika.
Wakati mvi zikiwa hazijatapakaa vichwani mwetu sababu ya uzee, ni vyema basi sisi tukajipanga vyema na kikamilifu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunauthaminisha uhuru wetu kwa kuufanya uendane na mamilioni ya Watanzania na sio genge la wateule wachache na vibaraka wao.
Alamsiki
2 comments December 29, 2006
KUMRADHI……KUMRADHI……KUMRADHI
Wapendwa wasomaji wangu, napenda kuwaomba radhi kwa usumbufu wowote mtakaoupata katika kipindi cha siku mbili tatu pindi mtakapokuwa mkitembelea blogi hii. Kuna matengenezo ya kiufundi yenye lengo la kuboresha mambo katika kijiwe hiki ambayo yanaendelea. Matengenezo haya yatakamilika ndani ya siku mbili. Nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu na nawaomba tena radhi kwa usumbufu mtakaoupata katika siku hizi mbili.
1 comment December 28, 2006
Sababu nakupenda rais wangu
Ni kwasababu ninakupenda mheshimiwa Raisi wangu ndio maana kwakweli nilijitahidi sana kukaa kando ya karedio kangu nikisikiliza jinsi ulivyokuwa “unachemka” kushusha mistari iliyokuwa imejaa vina juu ya kile kilichojiri ndani ya siku zako miatatu sitini na ushee hivi ukiwa katika makazi yako ya Magogoni.
Inawezekana sikukuelewa sana au kuendana na kile ulichokuwa ukituambia kwa maana ya kuwa na mtazamo wa kile hasa kilichokuwa nafsini mwako ulipokuwa ukichemka pale Kilimani, lakini kwasababu nakupenda Rais wangu, angalau niliambulia maneno mawili matatu hasa pale mwishoni mwishoni uliposema “Tukiwaunga mtazidi kuchemka” na kisha wakati unatoka ndani ya jumba lile, nasikia Vijana au skauti wa Chama wakawa wanakuimbia kawimbo kazuuuri, eti “Tukupambe maua”
Inawezekana usinielewe kwakweli, lakini kwasababu nakupenda sana mheshimiwa Rais wangu, nisingelipenda “Tukupambe” maana tutakuumiza sana. Ndio, tutakupamba kwa lipi mheshimiwa? Kwa shada la maua yaliyojaa miiba ya dhiki na ufukara unaoendelea kututesa? Kwanini tukupambe kwa mapambo ya kukuumiza mheshimiwa?
Na ukumbuke pia kuwa shada hili utavishwa ukiwa kizani, hali ambayo huenda ikakuumiza sana kwasababu lenyewe tayari lina miiba ambayo ni hatari na yenye sumu, akikosea mtu na kukuvisha vibaya sababu ya kiza huoni kuwa tutakuwa tumesababisha mengine?
Ni kwasababu nakupenda sana mheshimiwa raisi wangu ndio maana nimeona nikupongeze kwa kutaka “Tuwaunge mkono ili mzidi KUCHEMKA” sababu umekuwa mkweli zaidi ya tulivyotarajia kwakweli. yaani mmechemka kweli kweli katika kipindi hiki, lakini sidhani kama uungwaji mkono mnaotaka utakuwa makini kama mlivyotarajia.
Tutawaungaje mkono mheshimiwa Rais tukiwa gizani, operesheni hiyo haiwezi kuwa na matunda mazuri kabisa, sana sana itakuwa ya kuwaumiza maana hamna atakayekuwa anajua afanyacho huko kwenye giza zaidi ya kuwa tu naye kachomeka mkono wake hujui una sindano yenye dawa nzuri ya kutibu au laa.
Na kwakweli mheshimiwa Rais, kwasababu nakupenda kiongozi wangu ninaona ni vyema nikueleze kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa hivi, mtazidi “Kuchemka” zaidi ya hapo hasa mlioko katika jiji la Dar es salaam, maana mtapoozwa na nini ikiwa hata nguvu ya kusababisha viyoyozi viwapooze mnapochemka haipo?
Ni kwasababu ninakupenda kiongozi wangu niliyekupigia kura (au kukupikia kula?), ndio maana ningelipenda kwakweli ikiwezekana tujiulize pamoja mambo machache sana yafuatayo:-
Kweli unania tukuunge mkono kwa ajili uzidi kutusokomeza kizani kwa kisingizio cha kuwa tulishawekwa uelekeo wa kusukumiwa huko toka nyuma? Yale makali yako wapi mheshimiwa? Ya kutowaonea aibu wale wote ambao wana nia ya kuturejesha enzi za kutawaliwa? Inamaana mkono umevunjika ndio maana kweli umeshindwa kuwakamata hawa jamaa zetu wa Richmond, ambao kila kukicha wamekuwa wakikuchokonoa kwenye macho?
Inamaana kuwa mikono imevunjika ndio maana mnashindwa kuidaka shilingi yetu kiasi kwamba kila kukicha inazidi kuserereka, kama alivyotamka mzee wa Nji hii, Bw. Mrema? Ina uzito gani shilingi yetu kiasi cha kushindwa kuishikilia walau pale ilipokuwa hadi kuiacha iendelee kuzama?
Kilimo chetu badi kimeendelea kuwa kile kile cha kuchimba udongo hapa na kurudisha nyuma, kilimo cha miaka nenda miaka rudi, kile kile ambacho ulikipigia kelele sana kuwa utakifanyia maboresho na nilitarajia kwakweli hiki nacho kingepewa semina elekezi ili kibadilike kiende mbele kwa kasi, nguvu na ari yako, sasa mbona bado tuko pale pale? Au kime-tuchemsha tumeshindwa kukigusa?
Inawezekana kabisa kuwa umesahau kidogo baadhi ya ahadi zako, na kwakuwa nakupenda sana mheshimiwa Rais wangu, nitaomba nikukumbushe juu ya ahadi yako wakati ule wa kampeni, ahadi ya kupambana na rushwa. Mbona sijawasikia wale vigogo waliotajwa katika makabrasha mbalimbali kuwa japo wameopandishwa kizimbani na kusomewa tu mashitaka?
Na wale wauza unga ambao walizua mjadala mkubwa sana Bungeni hivi wameishioa wapi? Si ninakumbuka kuwa ulituambia umeshapewa majina yao mheshimiwa? Maana hatujatajiwa hata kutajiwa kuwa ni akina fulani na fulani. Au kutoka awamu ya tatu mlirithi tu tatizo la umeme na ile sera ya Uwazi na Ukweli hamkuona umuhimu wake?
Ni kwasababu ninakupenda kwakweli mheshimiwa Rais wangu, ndio maana napenda nikukumbushe juu ya kurejesha kale kautaratibu ka awamu iliyopita, kautaratibu ka kila mwezi kutuambia walau kuwa mmekusanya nini mwezi huo na mkatumia katika nini na nini.
Na ni kwasababu ninakupenda mheshimiwa Rais wangu, ndio maana nimeona niishie hapa leo ila nikaribishe wananchi wako wengine nao waelezee mapenzi yao kwako.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Tubariki sisi sote
Add comment December 22, 2006
Siku chache baada ya Moto wa Mwanjelwa

PICHANI: ni mabaki ya ndege aliyokuwa amepanda mheshimiwa Akukweti baada ya kupata ajali katika kiwanja kidogo cha ndege jijini Mbeya.
Siku chache baada ya moto uliounguza “mikoba” ya waheshimiwa fulani fulani pale Mwanjelwa, na mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi za Kitanzania kwa baadhi ya wafanyibiashara, akaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Mheshimiwa Juma Akukweti, si akaja Mbeya kuona ukubwa wa madhara yaliyotokana na moto huo na kisha kuwapa pole waathirika wa janga hilo!!!
Alipokuwa anataka kuondoka siku hiyo jioni hali ya hewa ikakataa, haikuruhusu apae na ka-ndege kake, akalazimika kuondoka alfajiri ya kesho yake yaani siku ya Jumamosi ya tarehe 16/12/2006. Kwa bahati mbaya sana akakumbana na dhahama la aina yake, ka-ndege kake kakashindwa kumudu kuruka, kakaenda kuvamia nyumba za wakazi zipatazo tatu na kulipuka.
Mungu epushia mbali, mheshimiwa akanusurika japo alipata majeraha yenye kumpa maumivu makali hasa sehemu za kichwani, na yeye na timu ya waliokuwa kwenye ndege hiyo wakawahishwa hospitali ya rufaa ya mkoani Mbeya kwa matibabu.
Kweli uswahilini noma, unajua wazushi wakaanza kudai huko mitaani eti jamaa hakutoa pole bali kuwabeza waathiurika wa moto ule kwa kuwaambia “Tulishawaambia mhame hapa lakini”, kwahiyo?? Huku uswahilini wanadai eti ajali ilitokana na chuki za wakazi aliowapa ukweli kuwa walishaambiwa wahame hawakusikia ndio maana moto ukawafanya kitu mbaya.
i{content: normal !important}i{content: normal !important}i{content: normal !important}
4 comments December 16, 2006
Mbeya, Kunani paleeee, mbona kila kitu kinawaka?

Ilianza katikati ya wiki kama masihara vile, wakati woko kuu na kubwa mjini Mbeya na lililo maarufu pia lijulikanalo kwa jina la Mwanjelwa lilipowaka moto na maduka yanayokadiriwa kufikia 500 hivi, (Hata city hawana uhakika maana yalikuwa yakiibuka kila uchao bila hata vibali), na mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya bilioni tano zikiteketea katika moto huo.
Siku hiyo hiyo katika eneo la Iyunga, kilomita zaidi ya tano toka Mwanjelwa, noto ulilipuka yalipo maghala ya Cocacola. Na katika eneo la Mama John, kama km moja na nusu toka mwanjelwa, watoto wawili walipoteza maisha kutokana na hitilafu zilizotokana na umeme.
Ajabu sasa ni siku ya pili yake, ambapo jamaa wanaosadikiwa kuwa na asili ya kabila la Ukinga, eti walikuwa wakilia sio kwa kuunguliwa na mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha, bali kwa kuunguliwa na “mikoba” yao. Ama kweli vilio hutofautiana. Wengine wanalilia fedha na mali zao walizokuwa wamefungasha kwa ajili ya wateja wa krismass, wengine wanalilia Mikoba yao iliyoungua!!! Ni vituko Uswahilini.
Ajabu sasa i{content: normal !important}i{content: normal !important}i{content: normal !important}
Add comment December 16, 2006
